Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchini Bolivia, Bwana Ban azingatia umuhimu wa kutunza sayari ya dunia

Nchini Bolivia, Bwana Ban azingatia umuhimu wa kutunza sayari ya dunia

Mabadiliko ya tabianchi ni wazi, na ni lazima kutunza sayari ya dunia amekariri leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akiongea wakati wa Kongamano la Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Utunzaji wa uhai, linalofanyika mjini Cochabamba, nchini Bolivia.

Bwana Ban amesema utunzaji wa sayari ya dunia ni jambo la kimaadili, akiongeza kwamba ni lazima kubadilisha jinsi ya kutumia rasilimali za dunia.

« Tunapaswa kubadilisha chumi zetu na kuchukua fursa ya mustakhabali inayotumia gesi chafuzi kidogo. Hakuna mpango mbadala kwa sababu hakuna sayari ya dunia mbadala. Duniani kote, matokeo ya mabadiliko ya tabianchi ni wazi, na yanaongezeka. Ukame, moto, mafuriko, mmomonyoko wa ardhi. Theluji inayoyayuka. Sayari ya dunia inatuonya. »

Kadhalika amemulika umuhimu wa kuheshimu ujuzi wa watu wa asili kuhusu mazingira, akisema ujuzi huo ni sehemu ya urithi wa dunia. Aidha ameongeza kwamba ni lazima kupunguza tofauti za utajiri kati ya watu wa asili na wengine, wakati ambap lengo la malengo ya maendeleo endelevu ni kuhakikisha hakuna mmoja anayeachwa nyuma.