Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwekeza katika wasichana ni kunufaisha jamii nzima : Ban

Kuwekeza katika wasichana ni kunufaisha jamii nzima : Ban

Wasichana wote wanapaswa kupewa fursa wanaostahili ili wakuwe viongozi, wafanyabiashara na raia wa siku za usoni, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya mtoto wa kike.

Kwenye ujumbe wake kwa siku hiyo Katibu Mkuu amesema ili kuwezesha watoto wa kike ni lazima kuwasaidia kuepukana na ndoa na mimba za utotoni, ukeketaji, na vile vile kuwapatia elimu bora na kuhakikisha wanakuwa na afya nzuri na ujuzi kuhusu haki zao katika maswala ya afya ya uzazi.

Aidha Bwana Ban amesema mafanikio yakipatikana kwa ajili ya wasichana, ni jamii nzima iitanufaika, akiongeza kwamba malengo ya maendeleo endelevu SDGs ni fursa kutokomeza umaskini, ukatili na ubaguzi kwa wote.

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake UN Women Phumzile Mlambo-Ngcuka amesema wasichana wenye umri wa miaka kumi na tano bado wanakumbwa na changamoto nyingi, wengi wakiwa wameacha shule, wengine wakiwa hatarini kuambukizwa na virusi vya ukimwi na milioni 250 wakiwa wameshaolewa.

Kwenye ujumbe wake kwa siku hiyo, Bi Mlambo-Ngcuka amesema jitihada zao zote ni kwa ajili ya wasichana hawa na wa vizazi vijavyo.