Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maabara ya kwanza ya jenetiki ya mimea kwa chakula na kilimo yaidhinishwa

Maabara ya kwanza ya jenetiki ya mimea kwa chakula na kilimo yaidhinishwa

Wajumbe kutoka nchi 136 wanachama wa Mkataba wa Kimataifa kuhusu Rasilmali za Jenetiki kwa chakula na kilimo (ITPGRFA), wameidhinisha kuanzishwa kwa maabara ya kuweka maelezo kuhusu mbegu za mimea ya chakula, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Chakula na Kilimo, FAO.

Makubaliao hayo ya pendekezo la kuweka mfumo wa kimataifa wa ukusanyaji habari kutoka kwa mkataba wa FAO kuhusu mbegu, yamefikiwa wakati wa mkutano wa wiki nzima uliohitimishwa leo Oktoba 9 mjini Roma, Italia.

Mfumo huo unatoa maelezo muhimu kuhusu aina zote za mimea duniani ili kuunda aina zinazohimili mazingira magumu.

Taarifa ya FAO imesema, wakati mabadiliko ya tabianchi yanapoongezeka kwa kasi, ni muhimu kwa wakulima, wanasayansi, wazalishaji wa mimea na kampuni za sekta binafsi kuwa na uwezo wa kuzalisha aina mpya za mimea inayohimili vidudu, mafuriko, na ukame, ili kuendeleza viwango vya kutosha vya uzalishaji wa kilimo.

Ili kufanya hivyo, FAO imesema wanapaswa kujua ni nini kilicho wapi, na jinsi ya kukipata, jambo ambalo si rahisi kufanya sasa hivi.