Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS yaongezewa muda, Sudan Kusini yahoji ndege zisizo na rubani

UNMISS yaongezewa muda, Sudan Kusini yahoji ndege zisizo na rubani

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa kura 13 kati ya 15 za wajumbe wake, azimio kuhusu Sudan Kusini ambalo pamoja na mambo mengine linaongeza muda wa ujumbe wa Umoja wa mataifa nchini humo, UNMISS hadi tarehe 15 mwezi Disemba mwaka huu.

Azimio hilo namba S2015/654 pia linaelekeza UNMISS kusaidia utekelezaji wa makubaliano ya amani yaliyotiwa saini hivi karibuni baina ya pande kinzani nchini Sudan Kusini na ofisi za ujumbe huo zitumike kusongesha harakati za Muungano wa Afrika kuleta maridhiano nchini humo.

Halikadhalika ibara ya Kumi ambayo inamtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kupatia kipaumbele upelekaji wa watendaji wa UNMISS kwenye maeneo yaliyoidhinishwa kuimarishwa kijeshi ikiwemo helikopta na ndege zisizokuwa na rubani.

Mwakilishi wa kudumu wa Sudan Kusini kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Francis Deng pamoja na kuunga mkono azimio hilo akisema linalenga kuimarisha amani nchini mwake, amehoji ibara hiyo ya kumi ya kupeleka askari na ndege hizo akisema..

(Balozi Deng)

“Inasikitisha sana kuwa masuala ambayo serikali yaSudan Kusini imeweka bayana msimamo wake, yameridhiwa na azimio hili bila kuzingatia mtazamo wa serikali. Nagusia zaidi Ibara ya 10 inayogusia upelekaji wa ndege zisizo na rubani. Inafahamika bayana kuwa hayo ni masuala ya mzozano na serikali na kuyajumuisha bila ridhaa ya serikali ni kuleta utata na uwezekano wa kutokuwepo kwa makubalano na chuki wakati amani na maelewano ndio jambo linalotakiwa.”

Kwa upande wake mwakilishi wa kudumu wa Angola kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Ismael A. Gaspar Martins pamoja na kuunga mkono azimio hilo amesema..

(Balozi Martins)

“Suala la vikwazo linasalia kuwa nyeti na nadhani baraza hili linapaswa kushughulikia kwa makini ili lisije likaibua shari badala ya kusuluhisha tatizo.”

Nchi 13 ziliunga mkono azimio hilo lililowasilishwa na Marekani ilhali mbili ambazo ni Urusi na Venezuela hazikuonyesha msimamo wowote kwenye upigaji kura wa azimio.

Mwakilishi wa kudumu wa Venezuela kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Rafael Darío Ramírez Carreño, amesema hatua yao inazingatia uwepo wa vipengele kama vile vikwazo ambavyo amesema vinaweza ukosefu wa amani nchini humo ilhali Sudan Kusini inatakiwa usaidizi ili kutekeleza makubaliano ya amani.