Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio lapitishwa kukamata meli zinazosafirisha binadamu kiharamu huko Libya

Azimio lapitishwa kukamata meli zinazosafirisha binadamu kiharamu huko Libya

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mkutano kuhusu uendelezaji wa amani na usalama duniani ambapo limepitisha azimio la kudhibiti usafirishaji haramu wa binadamu na wahamiaji kutoka pwani ya Libya. Assumpta Massoi na taarifa kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Azimio hilo namba S/2015/768 pamoja na mambo mengine linapatia kibali nchi wanachama au vikundi vya kikanda kukagua meli zinazopita bahari kuu kando ya pwani ya Libya pindi wanapohisi kuwa zinasafirisha wahamiaji au binadamu kwa njia haramu.

Halikadhalika linaruhusu nchi au vikundi hivyo kukamata zinazothibitika kutumika kusafirisha kiharamu binadamu au wahamiaji kutoka pwani ya Libya na kwamba kibali hicho ni kwa mwaka mmoja tu tangu kupitishwa kwa azimio hilo hii leo.

Balozi Matthew Rycroft ni mwakilishi wa kudumu wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa ambaye ameunga mkono azimio hilo akisema hawawezi kukubali watu kujinufaisha na machungu ya wengine.

(Sauti ya balozi Rycroft)

Hebu nieleweke ndugu Rais! Hatua zozote zitakazochukuliwa zitazingatia misingi na ukomo uliopitishwa na azimio hilo, na kutumika tu dhidi ya wasafirishaji haramu na meli tupu.   Mhamiaji yoyote atakayepatikana wakati wa operesheni hizo, atakapelekwa Ulaya kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa.”