Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasaka hifadhi 19 wahamishiwa Sweden katika mpango mpya wa EU

Wasaka hifadhi 19 wahamishiwa Sweden katika mpango mpya wa EU

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi katika Umoja wa Mataifa, UNHCR limekaribisha kuanza kwa safari ya kundi la kwanza la wasaka hifadhi waliohamishwa kutoka Italia kwenda Sweden, chini ya programu mpya ya Muungano wa Ulaya, EU.

Kuondoka kwa kundi hilo kunaanzisha rasmi mpango wa uhamishaji kutoka Italia, na kutafuatiwa na safari nyingine wiki ijayo.

Melissa Fleming ni msemaji wa UNHCR, Geneva

“Kundi hilo la wasaka hifadhi 19, wakiwemo wanawake watano, wote raia wa Eritrea, limeondoka leo asubuhi katika safari iliyong’oa nanga uwanja wa ndege wa Ciampino, mjini Roma. Walikuwa wamewasili Sicily kwa boti katika wiki chache zilizopita, na wakakaguliwa wote katika kituo cha mapokezi cha Lampedusa, ambapo walikubali kuhamishiwa Sweden.”

Mpango wa EU wa uhamishaji unatarajia kuwahamisha watu 160,000 kutoka Italia kwenda Ugiriki na nchi nyingine za EU zinazoshiriki, na uliafikiwa na Baraza la EU.

UNHCR inashiriki katika mpango huo kwa kushirikiana na wadau katika kutoa taarifa na ushauri kuhusu utaratibu mzima wa uhamishaji.