Skip to main content

Vurugu ukingo wa Magharibi, Zeid aomba utulivu

Vurugu ukingo wa Magharibi, Zeid aomba utulivu

Utulivu katika ukingo wa magharibi wa mto Jordan utarejea iwapo tu haki za binadamu zitaheshimiwa, amesema leo Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, amenukuliwa akisema kwamba mashambulizi yameripotiwa kwenye maeneo hamsini tofauti kwa kipindi cha wiki moja tu na kuonya kwamba mvutano na ghasia zinazidi kuongezeka kwa kasi.

Amesema mvutano huo ni matokeo ya kutawaliwa kwa wapalestina kwa muda mrefu na kuongezwa kwa vizuizi dhidi yao, hasa katika maeneo ya msikiti wa Al-Aqsa.

Kamishna Zeid ameeleza wasiwasi wake kuhusu matumizi ya silaha za ukweli na jeshi la Israel dhidi ya Wapalestina wanaoandamana, akisema kwamba ni matumizi ya nguvu ya kupindukia.

Kwa mujibu wa ofisi ya haki za binadamu, wapalestina 134 wamejeruhiwa wakati wa maandamano tangu tarehe 28 mwezi uliopita wa Septemba, huku wengine 150 wakikamatwa na baadhi ya nyumba zikibomolewa na jeshi la Israel, Kamishna Zeid akilaani aina hiyo ya adhabu.