Skip to main content

Baraza la Usalama laambiwa mazingira Haiti ni shwari kwa uchaguzi

Baraza la Usalama laambiwa mazingira Haiti ni shwari kwa uchaguzi

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limekuwa na mjadala leo kuhusu hali nchini Haiti, ambapo pia limehutubiwa na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MINUSTAH. Taarifa kamili na Abdullahi Boru.

(Taarifa ya Abdullahi)

Akilihutubia baraza hilo mwanzoni, Mkuu wa MINUSTAH, Bi Sandra Honore amesema hali ya usalama imeendelea kuwa imara nchini Haiti, na kwamba uchaguzi ujao wa tarehe 25 Oktoba mwaka huu ni mtihani wa kupima uwezo wa polisi wa nchi hiyo kudumisha usalama.

Akieleza kutiwa moyo na maandalizi ya uchaguzi huo ujao, Bi Honore amesema kuna mabadiliko makubwa ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwezi Agosti mwaka huu, huku akizingatia kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya Haiti, Baraza la Uchaguzi limechukua hatua za kuwaadhibu watu wanaochochea ghasia za uchaguzi.

“Mnamo Agosti 19, wagombe 16 kutoka vyama mbalimbali vya kisiasa walizuiwa kushiriki katika uchaguzi, kufuatia kuhusika kwao na vitendo vya ghasia za uchaguzi. Onyo zilitolewa pia kwa vyama 17 vya kisiasa ambavyo wafuasi wao waliripotiwa kuchochea vitendo vya uhalifu na kuwatisha wapiga kura.”

Bi Honore ameliomba Baraza la Usalama liongeze muda wa mamlaka ya MINUSTAH kwa kipindi cha mwaka mmoja, ili kuipatia muda serikali ya Haiti wa kuimarisha mamlaka yake, na pia kuwezesha kuhamisha mamlaka kwa njia taratibu.