Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamishna Zeid atoa wito kali kwa serikali ya Mexico ipambane na uhalifu

Kamishna Zeid atoa wito kali kwa serikali ya Mexico ipambane na uhalifu

Nchini Mexico, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein amemulika matishio dhidi ya haki za binadamu nchini humo, alipoongea na waandishi wa habari mwisho wa ziara yake Mexico. Grace Kaneyia na taarifa zaidi.

(Taarifa ya Grace)

Kamishna Zeid, ambaye amekutana na Rais wa nchi hiyo Piña Nieto, viongozi mbali mbali, wanaharakati wa haki za binadamu , wahanga wa mateso na wawakilishi wa jamii,7 amesema hali ya ghasia Mexico inashtusha sana, huku akieleza kwamba zaidi watu 150,000 wameuawa kwa kipindi cha miaka kumi na watu 26,000 wametoweka tangu mwaka 2007, wakati ambapo hakuna hata vita nchini humo.

Ameeleza kwamba uhalifu kutoka kwa vikundi vya majambazi na wafanyabiashara wa madawa ya kulevya ni moja ya sababu ya hali hiyo, lakini pia ufisadi na ukatili kutoka kwa mamlaka za serikali akitoa wito kwa viongozi.

(Sauti ya Kamishna Zeid)

“Jumuiya ya kimataifa ina nia nzuri kwa Mexico, lakini hatimaye ni raia wa Mexico tu, hasa viongozi wake, ambao wanaweza kutatua shida zake. Serikali ambayo itafanikiwa kubadilisha sekta ya polisi, kuhakikisha sheria inafanya kazi, kupunguza idadi ya uhalifu, kufunga wahalifu na kuwalinda waliotengwa ndicho kinachohitajika na taifa. ”

Hata kivyo amepongeza serikali ya Mexico kwa jitihada zake katika kupambana na changamoto hizo, akiisihi kuendelea kushirikiana vizuri na taasisi za Umoja wa Mataifa ambao una nia nzuri ya kuisaidia nchi.