Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNHCR aomba wakimbizi wa Afghanistan wasisahaulike

Mkuu wa UNHCR aomba wakimbizi wa Afghanistan wasisahaulike

Kamishna Mkuu wa Shirika la kuhudumia Wakimbizi duniani UNHCR Antonio Guterres ameonya leo kwamba mzozo wa Afghanistan umesahaulika, huku akisema bado wakimbizi milioni 2.6 kutoka Afghanistan wanaoishi kwenye nchi 70 duniani.

Akiongea wakati wa mkutano wa kamati tendaji ya UNHCR kuhusu wakimbizi wa Afghanistan, Bwana Guterres amesema jamii ya kimataifa inapaswa kujali hali ya nchi hiyo, kwani ingekuwa hatari kutojali mzozo huo.

Aidha Bwana Guterres amezipongeza nchi za India na Pakistan kwa ukarimu wao katika kupokea idadi kubwa ya wakimbizi, na pia, serikali jumuishi mpya ya Afghanistan kwa jitihada zake.

Hata hivyo amesema bado usalama ni tatizo nchini Afghanistan, akitolea mfano wa shambulio la Kunduz, na kueleza kwamba bado watu milioni moja ni wakimbizi wa ndani nchini humo.

Kwa mujibu wa UNHCR, mzozo wa Afghanistan umekuwa wenye idadi kubwa ya wakimbizi katika historia, idadi yao ikiwa imewahai kufika milioni 6. Bado UNHCR inashughulikia utaratibu wa kuwarejesha makwao wakimbizi kwa hiari, watu 54,000 wakiwa wamerudi nchini humo mwaka huu.