Skip to main content

Lee Hoesung ateuliwa mwenyekiti wa IPCC, Ban Ki-moon atoa pongezi

Lee Hoesung ateuliwa mwenyekiti wa IPCC, Ban Ki-moon atoa pongezi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha uteuzi wa Lee Hoesung kutoka Jamhuri ya Korea kuwa mwenyekiti wa Jopo la Pamoja na serikali kuhusu mabadiliko ya tabianchi, IPCC.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake, Katibu Mkuu amesisitiza jukumu la IPCC katika kutathmini utafiti unaofanywa kuhusu mchakato wa mabadiliko ya tabianchi, akikariri matokeo ya ripoti iliyotolewa na IPCC mwezi Novemba mwaka uliopita, iliyoonyesha wazi jinsi shughuli za binadamu zinavyochangia katika mabadiliko ya tabianchi na tishio kubwa litokanalo nayo.

Bwana Ban ameongeza kwamba ripoti hiyo ya msingi imeonyesha pia aina mbali mbali za hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi na kujenga mustakhabali endelevu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira UNEP Achim Steiner amesema uongozi wa IPCC ni muhimu sana wakati wa kuelekea mkutano kuhusu mabadiliko ya tabianchi, COP21 utakaofanyika mjini Paris mwishoni mwa mwaka huu.