Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani mauaji ya mlinda amani wa MINUSCA

Ban alaani mauaji ya mlinda amani wa MINUSCA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amelaani kuuawa kwa mlinda amani wa ujumbe wa kuweka utulivu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA, hapo jana mjini Bangui.

Msafara wa magari ya MINUSCA uliokuwa ukitoka mji wa Damara kwenda Ngerengou (katika mkoa wa Ombella-Mpoko) ulishambuliwa na kikundi cha watu wenye silaha, yapata kilomita 55 kutoka Bangui.

Taarifa ya msemaji wa Ban imesema askari jeshi wa MINUSCA kutoka Burundi walijibu mashambulizi hayo, na ndipo mlinda amani mmoja akauawa na mwingine kujeruhiwa. Hapa ni msemaji wa Katibu Mkuu, Stephane Dujarric, akiongea na wanahabari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York.

“Katibu Mkuu analaani vikali mashambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa, na kutoa wito hatua zichukuliwe hima kuwafikisha waliotenda uhalifu huu mbele ya sheria. Amekariri wito wake kwa vikundi vyenye silaha vikomeshe mapigano na na kusalimisha silaha zao. Katibu Mkuu anakariri pia ahadi ya Umoja wa Mataifa kuunga mkono mamlaka za Jamhuri ya Afrika ya Kati katika juhudi za kupamba na uhalifu na kumaliza ukwepaji sheria, chini ya mamlaka ya MINUSCA.”

Ban ametuma risala za rambirambi kwa familia ya mlinda amani aliyeuawa, na kwa serikali na watu wa Burundi, na kumtakia aliyejeruhiwa nafuu haraka.