Skip to main content

Ban akaribisha uamuzi wa Marekani kuwaachia huru wafungwa wapatao 6,000

Ban akaribisha uamuzi wa Marekani kuwaachia huru wafungwa wapatao 6,000

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekaribisha uamuzi wa serikali ya Marekani kuwaachia huru wafungwa wapatao 6,000 kutoka magereza ya kitaifa ili kupunguza msongamano katika magereza na kuwapa ahueni kidogo watu waliopewa vifungo virefu kwa makosa yasiyo ya kikatili yanayohusu dawa za kulevya.

Msemaji wa Katibu Mkuu, Stephane Dujarric amewaambia waandishi habari mjini New York kuwa Ban amekaribisha mapendekezo yanayolenga kuwaachia huru mapema wafungwa zaidi ambao wanahudumu vifungo ambavyo vinazidi ukubwa wa makosa yao, ambayo kwa wingi yanahusu dawa.

“Katibu Mkuu amesema kuwa serikali zinapaswa kutumia vifungo tu kama hatua ya mwisho, na baada ya kufikiria adhabu mbadala. Kuwafunga watu kwa muda mrefu ni moja ya sababu za msongamano gerezani, ambao huchangia mazingira yanayoweza kuchukuliwa kama unyanyasaji au hata utesaji”

Aidha, Ban amesema kuwa, ili kulishughulikia suala la msongamano gerezani, baadhi ya serikali zinapaswa kubuni njia mbadala kwa vifungo, na kufanyia marekebisho sera za adhabu na sheria ili kutoa hukumu zinazolingana na makossa. Kwa mantiki hiyo, Dujarric ameongeza:

Zinapaswa zizingatiwe njia zinazoweza kutumiwa badala ya kuhalifisha na kuwafunga watu wanaotumia dawa za kulevya, kwa kujikita zaidi katika afya ya umma, kuzuia, kutibu na kutoa huduma.”