Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuzuia wapiganaji wa kigaidi kuvuka mipaka ni changamoto ya kimataifa : CTED

Kuzuia wapiganaji wa kigaidi kuvuka mipaka ni changamoto ya kimataifa : CTED

Kamati ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na ugaidi, CTED, imetoa leo ripoti yake ya pili kuhusu wapiganaji wanaovuka mipaka ili kujiunga na vikundi vya kigaidi.

Kwa mujibu wa ripoti hii, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimeimarisha mifumo yao ya kupambana na tishio hilo ambalo limebainiwa kuwa tatizo la kimataifa.

Akiongea na Redio ya Umoja wa Mataifa, Mkurugenzi Mtendaji wa kamati hiyo, Jean-Paul Laborde ameangazia mafanikio yaliyopatikana.

« Nchi na ukanda zimeimarisha mfumo wa viza za mpito, na hiyo ni jambo jema kwa sababu uhuru wa kutembea ukiwa mkubwa mno, wapiganaji wa kigaidi kutoka nje watasafiri bila kudhibitiwa. Jambo jema la pili ni kwamba tumeweza kudhibiti zaidi pasipoti, Jambo jema la tatu ni kwamba sekta binafsi inashiriki kikamilifu katika swala hili. Kwa mfano Youtube imeondoa video milioni 14 ambazo zilikuwa na mashaka au zikishabikia ugaidi kwa kipindi cha mwaka mmoja. »

Aidha amesema Jean-Paul Laborde bado kasi na ubunifu wa vikundi vya kigaidi vinazidia uwezo wa nchi za Umoja wa Mataifa wa kupambana navyo, vikitumia mitandao ya kijamii na Intanet.

Kwa ujumla, takriban watu 30,000 kutoka nchi mia tofauti duniani kote wameajiriwa na wamevuka mipaka ili kujiunga na vikundi vya kigaidi.