Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuhuma dhidi ya Ashe zimegusa suala la uaminifu kwa Umoja wa Mataifa: Lykketoft

Tuhuma dhidi ya Ashe zimegusa suala la uaminifu kwa Umoja wa Mataifa: Lykketoft

Rais wa 70 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Mogens Lykketoft amezungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani na kusema kuwa suala la rushwa halina nafasi yoyote kwenye Umoja huo.

Bwana Lykketoft amesema yeye binafsi anazingatia misingi ya maadili na uwazi na kwamba tuhuma dhidi ya Bwana Ashe limegusa kwa ukali uaminifu wa Umoja wa Mataifa kwa hivyo..

(Sauti ya Mogens)

“Ofisi yetu bila shaka itashirikiana na mamlaka yoyote inayohusika kushughulikia kesi hii. Sifahamu iwapo tuna uwezo wa kutoa ushirikiano wa kiwango hicho kwani ndio kwanza tumeanza kazi chini ya mwezi mmoja uliopita, lakini tuko tayari kushirikiana. Iwapo kutakuwepo na umuhimu wowote wa kupitisha maamuzi kuhusu mwenendo wa ofisi ya Rais wa Baraza kuu au Rais mwenyewe, au taratibu za kuweka taarifa wazi, itakuwa ni wajibu wa baraza kuu lenyewe.”

Alipoulizwa iwapo kuna watendaji wengine wa Umoja wa Mataifa waliohusishwa kwenye sakata hilo..

(Sauti ya Mogens)

“IWapo kuna watu wengi zaidi ndani ya Umoja wa Mataifa wanahusika na sakata hili, sina taarifa zozote kuhusu hilo, inaweza kufichuliwa wakati wa mchakato wa kesi mahakamani sasa.”

Ashe na watu wengine watano walikamatwa leo Jumanne asubuhi kwa tuhuma za rushwa.