Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban azidi kupazia sauti mzozo huko Mashariki ya Kati baina ya Israel na Palestina

Ban azidi kupazia sauti mzozo huko Mashariki ya Kati baina ya Israel na Palestina

Hali ya usalama inazidi kudorora kila uchao huko Yerusalem na ukingo wa magharibi wa mto Jordan ambapo hii leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema anasikitishwa sana na hali inavyoendelea.

Taarifa ya msemaji wake imemnukuu akisema kuwa matukio  yanaongezeka akikariri mapigano ya hivi karibuni yaliyosababisha vifo na majeruhi wakiwemo  wapalestina wanne akiwemo mvulana mwenye umri wa miaka 13.

Ban amesema matukio hayo ni dalili kuwa mambo yanazidi kushamiri na siku si chache yatashindwa kudhibitiwa.

Ametaka serikali ya Israel ichunguze matukio hayo ikiwemo iwapo matumizi ya nguvu yalikuwa sahihi au yalipita kiasi.

Katibu Mkuu amesema haamini iwapo ubomoaji wa nyumba za wapalestina au ujenzi wa makazi mapya ya Waisrael kwenye ardhi ya wapalestina utakuwa na faida yoyote zaidi ya kuchochea mvutano baina ya pande mbili hizo.

Hata hivyo amekaribisha azma ya wapalestina na waisrael kushirikiana kudhibiti ghasia ikiwemo kuimarisha ulinzi kwa pamoja.

Amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake uko tayari kushirikiana na pande hizo kujenga mazingira yatakayowezesha mashauriano ya dhati ya kuwa na mataifa mawili yanayoishi pamoja.