Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM yalaani kampeni ya kuwachafua nchini CAR

IOM yalaani kampeni ya kuwachafua nchini CAR

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM limekanusha leo madai ya silaha kupatikana kwenye ofisi zao mjini Bangui nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR

Taarifa hiyo ilitolewa leo baada ya ofisi ya IOM kushambuliwa mjini Bangui tarehe 27 Septemba na kampeni dhidi ya kashfa hiyo kuibuka kwenye mitandao ya kijamii, ikisema kwamba silaha zilihifadhiwa ofisini kwao.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Geneva, msemaji wa IOM, Joel Millman amesema madai hayo yanaweza kuhatarisha usalama wa wafanyakazi wa IOM waliopo nchini humo.

(Sauti ya Joel Millman)

“Tunataka kusisitiza kwamba hatujawahi kuwa na aina yoyote ya silaha kwenye makao makuu yetu. Tulikuwa na vifurushi takriban 35 vya usalama vikiwa ni jaketi na kofia za kuzuia silaha, ambavyo mashirika mengi ya kimataifa huwa navyo . Sasa vimepotea,na tunaamini kwamba majambazi wameviiba.”

Aidha IOM imeeleza kuwa majambazi hao wameiba vifaa vya msaada kwa nyumba 350, pamoja na vifaa vya ujenzi kwa miradi yao. Sanaa zilizoandaliwa na watoto 100 kwa ajili ya maadhimisho ya ufunguzi wa shule pia zimeharibiwa.

Kwa ujumla watu 200,000 walioathirika na vita nchini CAR wamesaidiwa na IOM tangu mwaka 2013