UNHCR na WFP nchini DRC yakumbwa na wimbi la wakimbizi kutoka CAR
Zaidi ya watu 2,000 wamekimbilia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kwa kipindi cha wiki moja kufuatia ghasia zilizoibuka tena nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.
(Taarifa ya Priscilla)
Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo kwa pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR na la Mpango wa Chakula WFP, ikisema kwamba wengi wao ni watoto na wanawake waliokimbia machafuko mjini Bangui.
UNCHR na WFP zimeeleza wasiwasi wao kuhusu uhaba wa fedha unaokumba mashirika hayo, ambapo ni asilimia 6 tu ya dola milioni 57 zinazohitajika kwa UNHCR mwaka huu zikiwa zimepatikana, huku nusu ya mahema yaliyojengwa kwenye kambi ya Mole iliyo mpakani mwa CAR yakiwa yameharibika baada ya tufani iliyokumba maeneo hayo mwezi Septemba.
Kwa ujumla zaidi ya watu 100,000 wameshasaka hifadhi DRC kutoka CAR.