Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO na UNAIDS zaboresha huduma za afya kwa barubaru

WHO na UNAIDS zaboresha huduma za afya kwa barubaru

Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la afya WHO na lile la huduma za ukimwi, UNAIDS umezindua viwango vipya vya huduma za afya kwa barubaru ambao ni kundi lenye umri kuanzia miaka 10 hadi 19.

Mashirika hayo yamesema huduma za sasa hasa zile za dharura na malezi zinawaengua vijana wa kundi hilo ambapo ni lazima wapate ridhaa ya wazazi wanaposaka huduma, mathalani dhidi ya Ukimwi, ugonjwa ambao unaongoza kwa kuua barubaru wengi barani Afrika.

Akizungumza mjini Geneva, Uswisi, Dokta Anthony Costello, ambaye ni Mkurugenzi wa huduma za uzazi, watoto na barubaru kutoka WHO amesema viwango hivyo vipya kwa nchi maskini na tajiri vitatoa fursa ya kuboresha afya ya kundi hilo kwa kuwa..

(Sauti ya Dokta Castello)

"Kwanza ni kwa serikali, kuwapatia viwango ambavo zinanaweza kutumia kuweka vigezo vya huduma kwa barubaru. Pili kuna muongozo mzuri wa utekelezaji  ambao unatoa maelekezo ya jinsi ya kutekeleza vyema kitaifa na kwa wilaya . Tatu kuna baadhi ya miongozo ya utekelezaji kwa watoa huduma wa afya ambayo watatumia  kufuatilia kile wanachokifanya."

WHO na UNAIDS yamezingatia kuwa ubarubaru ni kipindi ambacho siyo tu watu wanakuwa hatarini kupata magonjwa, bali pia ni kipindi muhimu cha kujenga tabia ya kijana, tabia ambazo zitakuwa na athari kwa afya yake siku za usoni.