Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malaria na homa ya uti wa mgongo vyaripotiwa kaskazini mwa Mali

Malaria na homa ya uti wa mgongo vyaripotiwa kaskazini mwa Mali

Nchini Mali, wadau wa kibinadamu wameripoti ongezeko la wagonjwa wa Malaria kwenye mikoa ya Gao, Timbuktu na Kidal wakati huu ambapo homa ya uti wa mgongo tayari imeshaua watu wawili kati ya wanane waliokuwa na ugonjwa huo.

Ofisi ya usaidizi wa kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, OCHA imesema tayari hatua zimeanza kuchukuliwa kwa kupeleka kliniki za kuhama kutoka eneo moja hadi lingine ili kusaidia wizara ya afya, WHO na wadau wengine kuendelea kutoa huduma kwa visa vilivyoripotiwa.

Halikadhalika OCHA imesema inaendelea na taratibu kubaini iwapo viwango ongezeko la idadi ya wagonjwa wa Malaria na homa ya uti wa mgongo linaweza kutangazwa kuwa kuanza kuenea kwa ugonjwa huo kufuatia uvumi ulioenea wa kuwepo kwa homa isiyotambulika eneo hilo.

Wakati huo huo, OCHA imesema maandalizi yanaendelea ili kuanza kampeni kubwa ya chanjo dhidi ya homa ya uti wa mgongo kwenye maeneo ya Timbuktu.