Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia Yerusalem: Ban azungumza kwa simu na viongozi

Ghasia Yerusalem: Ban azungumza kwa simu na viongozi

Kufuatia ghasia zinazoendelea huko Mashariki ya Kati kwenye mji wa Yerusalem, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon anatarajia kuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu baadaye leo wakati huu ambapo tayari amekuwa na mazungumzo  kwa njia ya simu na Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas jana jioni.

Akiongea na waandishi wa habari mjini New  York Marekani, msemaji wa Umoja wa Mataifa  Stephane Dujarric amesema ujumbe wa Katibu Mkuu kwa viongozi hawa wawili ni kwamba wote wanawajibika ili kuhakikisha utulivu kwenye eneo hilo na kuzuia hali isizidi kuwa mbaya.

Bwana Dujarric ameeleza pia wasiwasi wa Katibu Mkuu kuhusu hali iliyoko  Yerusalem akisema kwamba analaani mashambulizi dhidi ya waisraeli na wapalestina katika baadhi ya maeneo ya mji huo, akisema kwamba mashambulizi hayo ni dalili ya mweleko hatari.

Akizingatia umuhimu wa kutekeleza suluhu ya mataifa mawili, Bwana Dujarric amemnukuu Katibu Mkuu akisema

“Ameshtushwa sana na matangazo ya vikundi vya wanamgambo wa Palestina wakijivunia mashambulizi hayo, huku akiwasihi viongozi wote kulaani ghasia na uchochezi, kuendelea kuwa na utulivu na kufanya lolote liwezekanalo ili kuzuia hali kuwa mbaya zaidi.”