Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DAFI yaleta nuru kwa wakimbizi wa Afghanistan nchini Pakistani:UNHCR

DAFI yaleta nuru kwa wakimbizi wa Afghanistan nchini Pakistani:UNHCR

Mpango wa usaidizi wa mafunzo ya juu unaofadhiliwa kwa pamoja na shirika la kuhudumia wakimbizi duniani, UNHCR na serikali ya Ujerumani, DAFI unaendelea kubadili maisha ya wakimbizi wa Afghanistan ambao walishakata tamaa ya kusonga mbele kielimu.

Mpango huo ulioanza mwaka 1992 nchini Pakistani, unatoa fursa kwa wakimbizi maskini kuweza kujiunga na vyuo vikuu ambapo Mwakilishi wa UNHCR nchini humo Indrika Ratwatte amesema ni uwekezaji wenye manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Amesema kupitia elimu ya vyuo vikuu na vyuo vya ufundi wanufaika wanapata stadi za maisha zinazohitajika kubadili maisha yao.

Mmoja wa wanufaika ni Abdul Khalil ambaye baada ya kufaulu elimu ya sekondari huko Afghanistan na kukimbilia ukimbizi hakuweza kusonga mbele hadi alipopata usaidizi wa DAFI na sasa amehitimu shahda ya kwanza anapanga kusoma shahada ya uzamili.

Khalil ambaye sasa anasoma, na kufanya kazi kiwandani pamoja na kufundisha kwenye shule moja ya majimbo ya Balochistan nchini Pakistani,  amesema anachotaka kuona sasa kila  mtoto mkimbizi kutoka Afghanistan anapata elimu kwani ndiyo njia pekee ya kustawisha nchi yao iliyosambaratishwa kwa vita.

Tangu mwaka 1992, mpango wa DAFI umesaidia wanafunzi 1,200 wa Afghanistan.