Skip to main content

Rasimu ya kwanza ya mkataba mpya wa tabianchi yawasilishwa

Rasimu ya kwanza ya mkataba mpya wa tabianchi yawasilishwa

Juhudi za kufikia mkataba mpya wa dunia nzima kuhusu tabianchi, zimeimarishwa leo kupitia kutolewa kwa rasimu ya kwanza ya kina ya mkataba huo.

Rasimu hiyo imeandaliwa na wenyekiti wenza wa kikundi kazi cha jukwaa la Durban (ADP), ambacho kilipewa jukumu la kufanya mashauriano kuhusu mkataba wa Paris. Rasimu hiyo imepewa umuhimu mkubwa kama  msingi wa mashauriano  ya fungu la mkataba wa Paris kuhusu tabianchi.

Mbali na mkataba wa Paris, fungu hilo linajumuisha rasimu ya azimio kuhusu utekelezaji wa mkataba huo kuanzia mwaka 2020, na rasimu ya azimio kuhusu mtazamo wa kabla yam waka 2020.

Nick Nuttall kutoka UNFCCC  anaeleza ni nini umuhimu wa kutoa rasimu hiyo ya kwanza ya mkataba mpya kuhusu tabianchi.

Sauti ya Nuttall

“Serikali zinahitaji rasimu ya mkataba ambayo zinaweza kushughulikia, ili ziweze kuweka saini mjini Paris Disemba. Mwaka 2020 ndipo mkataba huo mpya utaanza kutekelezwa, na bado tuna miaka mitano kabla kufanya hivyo, na kila mwaka ambapo hatuchukui hatua, gesi zaidi chafuzi zinavushwa angani. Kwa hiyo sehemu ya fungu hili lililowasilishwa leo kwa serikali inahusu hatua za kuchukua kabla ya 2020.”

Awamu itakayofuata ya mashauriano kuhusu mkataba wa tabianchi ni kuanzia Oktoba 19-23, 2015, mjini Bonn, Ujerumani.