Azimio kuhusu Ukatili wa kingono wakati wa mizozo lamulikwa na UM kabla ya kutimiza miaka 15

Azimio kuhusu Ukatili wa kingono wakati wa mizozo lamulikwa na UM kabla ya kutimiza miaka 15

Ukatili wa kingono wakati wa mizozo ulikuwa mada ya mkutano uliofanyika leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa ukimulika aina mbali mbali za mateso yanayopitiwa na wanawake wakati wa vita na mizozo.

Akiongea wakati wa mkutano huo, Liesl Gerntholtz, mkurugenzi wa idara ya haki za wanawake kwenye Shirika lisilo la kiserikali la Human Rights Watch, amesema ukatili wa kingono ni ukiukaji mkubwa wa haki za wanawake.

Ametolea mfano wa vurugu zilizotokea nchini Kenya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007-2008 ambapo wanawake wengi waliteswa na kubakwa akisema wengi waliojifungua watoto baada ya kubakwa wakati ule bado wanabaguliwa na jamii.

Kwa upande wake Paivi Kannisto, mkurugenzi wa idara ya usalama na amani kwenye shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake, UN Women lililoandaa mkutano huo, amefafanua matokeo ya utafiti huru uliofanyika kuhusu swala hilo.

(Sauti ya Paivi Kannisto)

“Tathmini inatukumbusha umuhimu wa kuhakikisha kuwa wanawake wanawakilishwa kwenye kila ngazi ya mifumo ya sheria. Kwa kweli wanawake wakiwakilishwa matokeo yanaonekana. Kuna haja ya kuhakikisha kuwa haki za wanawake zinaheshimiwa kabla, katikati na baada ya mzozo. Kwa hiyo mifumo ya sheria inapaswa kuimarishwa na pia uelewa wa watu kuhusu haki zao na jinsi ya kudai haki zao.”

Lengo la utafiti huo lilikuwa ni kutathmini utekelezaji wa Azimio namba 1325 kuhusu wanawake, amani na usalama lililopitishwa na Baraza la Usalama mwaka 2000 na ambalo litajadiliwa na BAraza hilo mwezi huu.