Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhakika wa chakula Sudan Kusini wazidi kutwama:FAO

Uhakika wa chakula Sudan Kusini wazidi kutwama:FAO

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO linaendelea na operesheni ya kufikisha msaada wa vyakula kwenye kaya Elfu 60 katika majimbo ya Unity na Upper Nile nchini Sudan Kusini kutokana na uhaba wa chakula unakabili maeneo hayo.

FAO inasema uhaba huo unatokana na kwamba akiba ya chakula imeisha na wananchi hawajaweza kushiriki shughuli za kilimo au uvuvi kwa mwaka mzima kutokana na mapigano na mvua.

Kaimu mwakilishi wa FAO nchini Sudan Kusini Serge Tissot amesema ukosefu wa  usalama unakwamisha operesheni zao akitolea mfano kuwa kwa sasa uwepo wao kwenye eneo husika ni nusu saa tu muda unaotosha kukabidhi vifaa kwa wadau na kuondoka na hawana muda zaidi wa maelezo kwa wahusika.

Hadi tarehe Mosi mwezi huu, FAO ilishakabidhi vikasha Elfu 70 vya kuokoa maisha vikijumuisha kilo mbili za mbegu za aina mbali mbali za mboga na vifaa vya uvuvi.