Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani mashambulizi Nigeria na Afghanistan

Ban alaani mashambulizi Nigeria na Afghanistan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani mashambulizi ya mabomu nchini Nigeria yaliyotokea kwa siku mbili tofauti huko kwenye viunga vya mji mkuu wa Nigeria, Abuja na huko Maiduguri, mji mkuu wa jimbo la Borno nchini humo.

Yadaiwa mashambulio hayo yamefanywa na magaidi wa Boko Haram ambapo Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa huku akiwatakiwa ahueni majeruhi.

Ban amenukuliwa na msemaji wake akisema kuwa mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Boko Haram ni kinyume cha sharia za kimaitaifa, ubinadamu halikadhalika imani ya kidini.

Amesisitiza azma ya Umoja wa Mataifa ya kuendelea kusaidia serikali ya Nigeria katika kukabiliana na ugaidi huku akitaka uzingatiaji wa haki za binadamu wakati wa harakati dhidi ya ugaidi.

Wakati huo huo Katibu Mkuu amelaani vikali mashambulizi ya huko Kunduz, nchini Afghanistan, mashambulizi yaliyofanywa kwenye hospitali na kusababisha vifo vya watu kadhaa na wengine kujeruhiwa.

Hospitali hiyo inaendeshwa na shirika la madaktari wasio na mpaka, MSF ambapo Ban amekumbusha kuwa wahudumu wa afya wanapaswa kulindwa na hivyo uchunguzi wa tukio hilo la leo ufanyike haraka ili wahusika wawajibishwe.