Skip to main content

Walibya kataeni ghasia na hima mhitimishe mazungumzo- Ban

Walibya kataeni ghasia na hima mhitimishe mazungumzo- Ban

Leo hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, umefanyika mkutano wa ngazi ya juu kuhusu Libya, ukiwaleta pamoja Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi tano, zikiwemo Marekani, Misri , Italia, Morocco na Uturuki.

Katika hotuba yake, Katibu Mkuu Ban Ki-moon amewaambia wawakilishi wa Libya kuwa jamii ya kimataifa inaunga mkono juhudi za pamoja za Walibya kuchagua amani badala ya ghasia, na ustawi badala ya vurugu.

“Kwa upande wenu, ni lazima mkatae machafuko na kuhitimisha mazungumzo bila kuchelewa. Kila mmoja wenu ana uwezo wa kujenga Libya mpya na kuisongesha nchi mbele kupitia serikali ya mkataba wa kitaifa.”

Ban amesema ni katika umoja tu ndipo Walibya wanaweza kutumainia kujenga nchi inayoonyesha moyo wa mapinduzi na kuwaenzi waliojitoa kupigania mapinduzi hayo. Ban amesema hakuna muda wa kupoteza..

“Nimemwelekeza mwakilishi wangu maalum atimize ratiba iliyokubaliwa ya kuanza mazungumzo wiki hii kuhusu kuundwa kwa serikali mpya”