Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ana taarifa kuwa Urusi imeanza mashambulizi ya anga huko Syria

Ban ana taarifa kuwa Urusi imeanza mashambulizi ya anga huko Syria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ana taarifa kuwa Urusi imeanza mashambulio ya anga karibu na mji wa Homs na kwingineko nchini Syria.

Msemaji wa Umoja huo Stephane Dujarric amesema hayo alipoulizwa na waandishi wa habari jijini New York, kuhusu taarifa za mashambulizi hayo na iwapo yatasaidia kumaliza mzozo unaoendelea nchini humo.

Bwana Dujarric amesema wanaelewa kuwa hatua hiyo inafuatia ombi la serikali ya Syria na taarifa za awali zinataja kuwepo kwa majeruhi karibu 33 ambao ni raia huko Homs.

Amemnukuu Bwana Ban akisisitiza kuwa mashambulizi yanayofanywa na nchi yoyote au upande wowote huko Syria lazima yazingatie sheria za kimataifa za kibinadamu na kwamba hatua zozote za kuepusha raia dhidi ya zahma hiyo lazima zipatiwe kipaumbele.

Ametaka uchunguzi wa matukio hayo ya raia kujeruhiwa kutokana na mashambulizi ya anga Syria na kwamba bila mshikamano wa dhati wa kimataifa wa kupatia suluhu mzozo huo, haitakuwa rahisi kuumaliza na hatimaye kutokomeza kundi la ISIL au Daesh.