Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nipo tayari kuanza mazungumzo mara moja na Palestina, bila masharti- Netanyahu

Nipo tayari kuanza mazungumzo mara moja na Palestina, bila masharti- Netanyahu

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, amesema yupo tayari kuanza mazungumzo ya amani mara moja na Palestina, iwapo Palestina itataka kushiriki, bila masharti.

Bwana Netanyahu amesema hayo leo Alhamis akilihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, katika mjadala wa wazi wa kikao cha Baraza hilo cha 70.

Netanyahu amesema sasa ni wakati wa kuchukua hatua kwa ajili ya watu wa Palestina na Israel

“Nipo tayari kurejelea mara moja mazungumzo ya moja kwa moja ya amani na mamlaka ya Palestina bila masharti yoyote asilani. …Rais Abbas, najua si rahisi. Najua ni vigumu, lakini watu wetu wanatudai kuendelea kujaribu, kwa sababu kwa pamoja, tukijaribu kuketi chini na kujaribu kuutatua mzozo huu kati yetu, na kutambuana, tunaweza kuwafanyia watu wetu mambo makubwa.”

Aidha, Netanyahu ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa uitendee Israel haki, akimulika maazimio yaliyopitishwa na Baraza Kuu dhidi ya Israel

“Umoja wa Mataifa unaweza kusaidia kuendeleza amani kwa kuunga mkono mazungumzo ya moja kwa moja bila masharti kati ya pande kinzani. Umoja wa Mataifa hautaweza kuendeleza amani kwa kujaribu kulazimu suluhu au kwa kuunga mkono kukataa kwa Palestina. Na wajumbe waheshimiwa, Umoja wa Mataifa, hatimaye unapaswa kuacha mara kwa mara kuikemea Israel.”