Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wasisitiza umuhimu wa kuheshimu utu wa wakimbizi na wahamiaji

Umoja wa Mataifa wasisitiza umuhimu wa kuheshimu utu wa wakimbizi na wahamiaji

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema mzozo wa uhamiaji na ukimbizi unaokumba dunia sasa ni mkubwa zaidi katika historia yake tangu vita vikuu vya pili.

Akizungumza kwenye mkutano wa ngazi ya juu kuhusu uhamiaji na ukimbizi uliofanyika leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Bwana Ban amesema kwamba jamii ya kimataifa inapaswa kuwajibika ili kupata suluhu kwa kuheshimu haki za binadamu, akieleza:

(Sauti ya Ban)

“ Tunapaswa kuongeza bidi ili kuzuia na kukomesha vita na mateso. Lakini tunajua kwamba mizozo haitaisha mara moja. Watu zaidi watakimbia vita, na watu wataendelea kuhama ili kutafuta fursa bora. Tunapaswa kujitayarisha zaidi.”

Ametoa mapendekezo manane katika suala hilo, yakiwemo haki ya wakimbizi kuhudumiwa kwa heshima na utu, haki yao ya kusaka hifadhi, umuhimu wa kuongeza nafasi za mapokezi, na fursa za uhamiaji halali.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, Antonio Guterres, amesisitiza kwamba mwelekeo kwenye miaka ya baadaye ni kuendelea kuongezeka kwa idadi ya watu wanaokimbia nchi zao kutokana na vita, mabadiliko ya tabianchi na upungufu wa usaidizi wa kibinadamu.

Hata hivyo Bwana Guterres amezingatia kwamba wakimbizi ni binadamu ambao wanapaswa kuheshimiwa, akiongeza kwamba nchi zinapaswa kuwajibika na kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu.