Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Israeli ikikiuka makubaliano, nasi hatutatekeleza peke yetu: Rais Abbas

Israeli ikikiuka makubaliano, nasi hatutatekeleza peke yetu: Rais Abbas

Rais Mahmoud Abbas wa mamlaka ya Palestina, ametoa wito kwa nchi zinazosema kuwa zinaunga mkono suluhu ya mataifa mawili kwa mzozo baina ya Palestina na Israel, zitambue pia Palestina kama taifa, sio Israel pekee.

Rais Abbas amesema hayo akilihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, katika mjadala wa wazi wa kikao cha 70 cha baraza hilo.

Akishukuru Ufalme wa Sweden na nchi kadhaa za Ulaya zilizotambua utaifa wa Palestina, Rais Abbas amesema

(Sauti ya Abbas)

“Leo natoa wito kwa nchi ambazo hazijatambua taifa la Palestina bado, zifanye hivyo. Tuna Imani kuwa zitafanya hivyo, kwa misingi ya haki wanayostahili watu wetu na ndoto yao.

Amegusia pia vitendo vya uvamizi wa mara kwa mara dhidi ya msikiti wa Al Aqsa huku ambapo amesema wavamizi wanazuia waumini wa kiislamu kuingia msikitini kwa ajili ya ibada akisema kitendo hicho kitabadili mzozo wa sasa kutoka wa kisiasa kuwa wa kidini.

Amesema jamii ya kimataifa haichukui hatua dhidi ya vitendo vinavyofanyiwa wapalestina ikiwemo kuchomwa moto maeneo ya ibada na hivyo akahoji..

(Sautiya Abbas)

“Je ni kwa muda gani Israel itaendelea kuwa juu ya sheria ya kimataifa bila kuwajibishwa?”

Na ndipo akarejelea hatua ya kupandishwa kwa bendera ya Palestina kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa akishukuru nchi ambazo ziliunga mkono azimio la kuwezesha kupandishwa kwa bendera ya Palestina kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa akisema..

“Wakati hauko mbali tutakapopandisha bendera ya Palestina huko Yerusalem Mashariki, mji mkuu wa Palestina.”

Rais Abbas amesema iwapo Israel itaendelea kukiuka makubaliano kati yao, Palestina nayo haitakubali kusalia yenyewe kuyatekeleza peke yake akieleza kuwa huo ni uamuzi uliopitishwa na bunge la Palestina.