Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu ndio ufunguo wa mabadiliko katika usawa wa jinsia- Rais Mahama

Elimu ndio ufunguo wa mabadiliko katika usawa wa jinsia- Rais Mahama

Rais John Mahama wa Ghana, amesema leo kuwa tatizo la kutokuwa na usawa wa kijinsia linaweza kupatiwa mwarobaini iwapo mizizi yake itashughulikiwa, akiongeza kuwa elimu ndio ufungua wa kutimiza lengo la kufikia usawa wa jinsia.

Rais Mahama amesema hayo wakati akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, katika mjadala wa wazi wa kikao cha 70.

Rais Mahama amesema kuwa baada ya bara Asia, bara la Afrika ndilo lenye viwango vya juu zaidi vya ndoa za utotoni,

“Lakini utafiti umeonyesha kuwa asilimia 64 ya wasichana wataepushwa ndoa za utotoni ikiwa wataruhusiwa kumaliza shule ya sekondari.”

Kuhusu kufanyia marekebisho mfumo wa Umoja wa Mataifa, Rais Mahama amesema wakati wa kufanya marekebisho hayo ni sasa ili mfumo huo uwe jumuishi zaidi.

“Ukweli ni kwamba, wakati huo umepita kitambo. Ulimwengu uliokuepo mwaka 1945 haupo tena sasa. Kwa hiyo, Umoja wenye maono ulioundwa kukidhi mahitaji ya ulimwengu huo, ni lazima sasa ufanyiwe marekebisho ili ukidhi mahitaji ya ulimwengu wa sasa.”

Kuhusu masuala ya ubaguzi, wakimbizi, na ulinzi wa amani, Rais Mahama amesema

“Wakati kabila moja la wananchi wanapohisi uhai wao haufai, wakimbizi wanapokimbia ukatili wa vita, na hatimaye kukutana na ukatili katika nchi za ng’ambo, watu walio katika uchungu wa vita wanaponyanyaswa na walinda amani wa kimataifa waliopelekwa kuwalinda, hapo sisi kama viongozi na jamii ya kimataifa, ni lazima tukomeshe ukimya na kuchukua hatua”.