Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akutana na mawaziri wa Nje wa P5, kuhusu Syria, Yemen na Sudan Kusini

Ban akutana na mawaziri wa Nje wa P5, kuhusu Syria, Yemen na Sudan Kusini

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekutana na kufanya mazungumzo na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama, yaani P5, ambapo wamemulika masuala ya Syria, Yemen na Sudan Kusini.

Katika mkutano huo na mawaziri John F. Kerry wa Marekani, Wang Yi wa Uchina, Laurent Fabius wa Ufaransa, Philip Hammond wa Uingereza na Sergey V. Lavrov wa Urusi, Katibu Mkuu amesema nchi hizo wanachama wa P5 wa Baraza la Usalama wana umuhimu mkubwa katika juhudi za kupatia suluhu mizozo ya nchi hizo tatu.

Taarifa ya msemaji wake imesema Ban ameeleza kutegemea kujituma kwa nchi hizo kama wanachama wa P5 kufikia msimamo wa pamoja, ambao unahitajika kuutanzua mzozo wa Syria.

Kuhusu Yemen, Ban amesisitiza masikitiko yake makubwa kuhusu mzozo mkubwa wa kibinadamu, pamoja na idadi inayoongezeka ya wahanga wa kiraia katika mapigano, hususan kutokana na mashambulizi ya angani.