Zeid ataka pande zote katika mgogoro Afghanistan kulinda rai

Zeid ataka pande zote katika mgogoro Afghanistan kulinda rai

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad Al Hussein ameelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu hali ya haki za kibinadamu katika mji wa Kaskazini Mashariki wa Kunduz nchini Afghanistan, kufuatia shambulizi kubwa la jana lilitokelezwa na kundi la Taliban.

Katika taarifa, Kamishna Zeid ametoa wito kwa pande zote katika mgogoro  huo kuchukua hatua zote za kuwalinda raia dhidi ya madhara.

Kamishna huyo amesema, raia wa Kunduz tayari wameteseka kufuatia mapigano ya miezi kadhaa, na sasa wako katika hatari kubwa, ishara ya kuongezeka kwa mzozo.

Kama njia ya kutuliza hali, Kamishna Zeid amesihi pande zote katika mgogoro huo kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya haki za kibinadamu ya kuwalinda raia na kuchukua hatua zozote yakinifu ili kulinda maisha na kuzuia kujeruhiwa kwa raia.