Adhabu ya kifo si faraja kwa familia za wahanga: Zeid

30 Septemba 2015

Asilimia 82 ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wametangua au hawatumii tena adhabu ya kifo, ikiwa ni ongezeko kubwa tangu kuanzishwa kwa Umoja huo ambapo nchi 14 tu zilikuwa hazitumii adhabu hii.

Hii ni kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Zeid Ra’ad al Hussein, akihutubia kikao kuhusu adhabu ya kifo kwa niaba ya Katibu Mkuu, kilichofanyika leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Kamishna Zeid amesema licha ya mafanikio makubwa, baadhi ya nchi ulimwenguni zimeongeza adhabu za kifo kwa kipindi cha miezi michache iliyopita, zikichukua kisingizio cha haki za familia za wahanga.

(Sauti ya Zeid)

“Kwa ukweli, familia nyingi za wahanga wa mauaji wanaamini kwamba kujibu kwa mauaji na mauji si heshima kwa wahanga. Kwenye nchi nyingi duniani kote, wahanga wa mauaji ya kutisha, yakiwemo mauaji ya kimbari, ya kivita na ugaidi wamepigia chepuo kusitishwa kwa  adhabu za kifo”  

Akihutubia mkutano huo, waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Louise Mushikawabo ameeleza kwa nini nchi yake iliamua kutangua adhabu ya kifo mwaka 2007 ili kulinda haki ya msingi ya uhai na kukuza maridhiano nchini humo, ingawa mwanzoni wananchi walipinga uamuzi huo na ilibidii waelimishwe na uongozi.  

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud