Raia wauawa wakisherehekea harusi Yemen, Ban alaani

Raia wauawa wakisherehekea harusi Yemen, Ban alaani

Nchini Yemen, watu wapatao 135 wameuawa baada ya kushambuliwa kwa maroketi ya angani wakati wakiwa kwenye sherehe ya harusi katika kijiji kimoja cha mjini Mokha.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani shambulio hilo, akinukuliwa akituma rambirambi kwa familia za wafiwa huku akiwatakia ahueni majeruhi.

Ban amerejelea wito wake wa mara kwa mara kuwa hakuna suluhu ya kijeshi kwenye mzozo wa Yemen na kwamba mashambulizi yanayoendelea yanazidisha machungu kwa wananchi na uharibifu wa nchi hiyo.

Katibu Mkuu ametaka pande husika kwenye mzozo huo ziwe za ndani au nje ya nchi zisitishe shughuli zao za kijeshi na kumaliza tofauti zao kwa njia ya mazungumzo.