Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuishinda ISIL katika mbuga za vita haitoshi- Obama

Kuishinda ISIL katika mbuga za vita haitoshi- Obama

Rais Barack Obama wa Marekani, amesema haiotoshi kulishinda kundi linalotaka kuweka Uislamu wenye itikadi kali, ISIL, katika mbuga za mapigano tu.

Rais Obama amesema hayo wakati wa mkutano wa viongozi kuhusu kukabiliana na ISIL na itikadi kali katili, ambao umefanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, kama sehemu ya mikutano ya Baraza Kuu la 70.

Obama amesema hatua ya kwanza ni kuzuia ISIL kushawishi, kusajili na kuwahamasisha wengine kufanya ukatili

“Hii inamaanisha kushinda dhana zao. Dhana hazishindwi kwa bunduki, zinashindwa kwa mawazo bora zaidi, na mitazamo inayovutia na kushawishi.”

Aidha, Rais Obama amesema anatambua kuwa hawana budi kukabiliana na malalamiko ya kiuchumi yanayo yaliyopo katika maeneo ambayo ISIL inataka kusingizia

“Umaskini hausababishi ugaidi, lakini tulivyoona Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, watu, hususan vijana, wanapofanywa kuwa maskini na bila matumaini, na wakahisi wanadhalilishwa kwa kunyanyaswa na ufisadi, hayo yanaweza kuibua chuki, ambayo magaidi wanadakia. Ndio maana maendeleo endelevu, kufungua fursa na utu, hususan kwa vijana, ni sehemu ya kukabiliana na itikadi kali katili.”

Mengine ambayo Obama ametaja kama mambo yanayowezesha propaganda ya kigaidi kunawiri na kuchochea ukatili, ni kunyima watu haki zao na kutowapa fursa ya kujieleza kwa amani, pamoja na kuwachukulia wapinzani wa kisiasa kama magaidi na kuwatupa gerezani.