Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dhamira yetu ni kuzuia ukatili wa itikadi kali, zaidi ya kukabiliana nao- Ban

Dhamira yetu ni kuzuia ukatili wa itikadi kali, zaidi ya kukabiliana nao- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema vikundi katili vya itikadi kali, vikiwemo Da’esh na Boko Haram, ni tishio la moja kwa moja kwa usalama wa kimataifa, vikilenga wanawake na wasichana kinyama na kudunisha maadili ya ujumla ya amani, haki na utu wa mwanadamu, na kwamba tishio hilo linazidi kukua.

Ban amesema hayo katika mkutano wa viongozi kuhusu kukabiliana na kundi la linalotaka kuweka dola la Uislamu wenye itikadi kali, ISIL na itikadi kali katili kwa ujumla, ambao umesimamiwa na Rais Barack Obama.

Katibu Mkuu amesema kushughulikia changamoto hii ni jambo lililo kwenye kiini cha kazi ya Umoja wa Mataifa, na kwamba linahitaji jitihada za pamoja.

“Tunajua itikadi kali katili hunawiri pale haki za binadamu zinapokiukwa, hamu ya kujumuishwa inapopuuzwa, na pale watu wengi mno, hususan vijana na matumaini na ndoto zao, wanapokosa fursa na maisha yenye maana. Tunajua pia kinachohitajika kwa ufanisi: Utawala bora. Utawala wa sheria. Jamii zenye dhana tofauti na uwazi. Elimu bora na ajira zenye hadhi. Kuheshimu kikamilifu haki za binadamu.”

Ban amesema hatua za kiusalama za kukabiliana na ugaidi ni muhimu

“Lakini hatuwezi kuacha juhudi hizo zikafeli kwa kuwapa nguvu wale tunaonuia kushinda, au kwa kuwatenga hata zaidi vikundi au jamii za watu waliotelekezwa tayari. Dhamira yetu ni lazima twende hatua zaidi ya kukabiliana ukatili wa itikadi kali, na kwanza kuuzuia.”