Skip to main content

Ban na Mashirika ya Kimataifa walaani vurugu CAR

Ban na Mashirika ya Kimataifa walaani vurugu CAR

Vurugu zimeripotiwa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ambapo watu zaidi ya 30 wameuawa na wengine zaidi ya 100 wamejeruhiwa kwenye mji mkuu Bangui. Tayari Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amelaani mlipuko huo wa ghafla wa vurugu kama anavyoelezea Amina Hassan katika ripoti hii.

(Taarifa Kamili na Amina Hassan)

Katika taarifa, Katibu Mkuu amelaani vikali vitendo vyote vya vurugu na kutoa wito wa kusitishwa haraka kwa vurugu na mashambulizi ya kulipiza kisasi. Vurugu hizo zimetokea baada ya kijana wa dhehebu la kiislamu kuuawa mjini Bangui ambapo Ban amesihi mamlaka ya mpito nchini kufanya kila liwezalo kuzuia ghasia zaidi. Tayari shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa nalo linasaka uwezekano wa kufikia maelfu ya watu wanaokimbia mji huo huku ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ikisema ina wasiwasi na hali ya sasa.

Rupert Colville ni msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa:

(SAUTI COLVILE)

“ Nadhani hali hii inaonyesha watu wanarejea kwa idadi kubwa na hali hiyo inaweza kugeuka kuwa janga CAR. Takwimu za watu waliofurushwa zinaelezea hali halisi, ukweli kwamba watu wapya wanaendelea kufurushwa makwao na kuna ufyatulianaji wa risasi katika mjii mkuu, kando na maeneo ya vijijini, inatia wasiwasi kwa ukweli."

Kwa mujibu wa UNHCR watu wasiopungua 27,400 wamekimbia makazi yao, ikiwa ni pamoja na wengine 10,000 ambao walikuwa wanaishi katika eneo la Mpoko lililoko karibu na uwanja wa ndege ambao tayari ulikuwa na watu 11,000.