Skip to main content

Sudan Kusini yamulikwa kando ya #UNGA

Sudan Kusini yamulikwa kando ya #UNGA

Mkutano wa ngazi ya juu kuhusu Sudan Kusini umefanyika leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa MAtaifa Ban Ki-moon amewasihi viongozi wa nchi hii kurekebisha makosa yao na badala yake kujali raia waliowachagua. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Akihutubia kikao hicho, Bwana Ban amekariri msimamo wa Umoja wa Mataifa wa kusaidia Sudan Kusini, akiwaomba viongozi kuheshimu makubaliano ya amani yaliyosainiwa mwezi uliopita akisema :

« Sudan kusini iko njia panda. Njia iliyo mbele yetu ni ngumu. Nawasihi waliosaini makubaliano watimize ahadi zao na kutekeleza makubaliano bila kuchelewa. Haiwezekani tena kurejea vitani.”

Kwa upande wake Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amesema tayari jitihada zao zimekuwa nyingi.

(Sauti ya Sala Kiir)

“ Leo nakariri mbele yenu msimamo wangu wa kuhakikisha utekelezaji thabiti wa makubaliano hayo, nawajibika kikatiba na kimaadili kurejesha amani na maendeleo kwa watu wangu ambao wameteseka kwa zaidi ya miaka hamsini kutokana na vita vya ukombozi dhidi ya utumwa, ubaguzi na ukosefu wa maendeleo.”