Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jamii ya kimataifa yatoa ahadi kwa ajili ya hatma ya Somalia

Jamii ya kimataifa yatoa ahadi kwa ajili ya hatma ya Somalia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema Somalia imepiga hatua kubwa katika ujenzi wa taifa na demokrasia akisihi viongozi wa nchi hiyo kuendelea kuonyesha bidii ili kuboresha utawala wa sheria kupitia uchaguzi jumuishi ifikapo mwaka 2016.

Bwana Ban amesema hayo kwenye mkutano wa ngazi ya juu kuhusu Somalia uliofanyika leo sanjari na kikao cha 70 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Akizungumzia tishio la Al-Shabaab, Katibu Mkuu amesema suluhu dhidi ya kundi hilo la kigaidi siyo tu ya kijeshi.

(Sauti ya Ban)

“Tunapaswa kuelewa sababu zinazovutia watu kujiunga na Al-Shabaab. Tunapaswa kusaidia mamlaka za Somalia kuunda suluhu mbadala, ikiwemo kujenga taifa jumuishi, usalama, haki na fursa za kiuchumi kwa wote, kwa kuheshimu haki za binadamu kwa wote na kuwezesha wanawake wa Somalia.”

Aidha akisema bado watu zaidi ya 800,000 wanakosa chakula cha kutosha nchini Somalia, Bwana Ban ametoa wito kwa ufadhili wa kimataifa.

Kwa upande wake Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud amemulika mafanikio yaliyopatikana nchini Somalia kwa kipindi cha miaka minne, katika sekta ya usalama na jitihada za kuunganisha nchi.