Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi waahidi kuimarisha mfumo wa ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa

Viongozi waahidi kuimarisha mfumo wa ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa

Katika kikao maalum kuhusu operesheni za ulinzi wa amani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ni wakati sasa wa kuleta mabadiliko katika mfumo huo, akitaja ni lazima kuongeza uwezo wa kijeshi, polisi na kuwa na vikosi vya akiba.

Halikadhalika amemulika umuhimu wa kupambana na ukatili wa kingono unaofanywa na walinda amani.

Kwa upande wake Rais wa Rwanda Paul Kagame ameahidi kutoa helikopta Mbili, hospitali mbili na walinda amani 1,600 pamoja na kikosi kizima cha polisi wa kike, akisisitiza uwajibikaji na uaminifu katika operesheni za ulinzi wa amani.

Naye Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema nchi yake inaweza kuchangia kiasi chochote cha walinda amani, iwapo ufadhili utapatikana, akiahidi kuchangia vikosi viwili vya ziada vya walinda amani.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, nchi 120 zinachangia katika operesheni za amani za Umoja wa Mataifa, ambazo zinahusisha walinda amani 120,000. Kwa ujumla idadi ya wanajeshi walioongezwa kutokana na ahadi zimetolewa kwenye mkutano huo ni zaidi ya 30,000.