Skip to main content

Tusipochukua hatua Paris mwezi Disemba, sayari ya dunia iko mashakani: François Hollande

Tusipochukua hatua Paris mwezi Disemba, sayari ya dunia iko mashakani: François Hollande

Akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais wa Ufaransa François Hollande amesisitiza umuhimu wa mkutano kuhusu mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika Paris mwezi Disemba mwaka huu akisema viongozi watapaswa kuchukua hatua, pengine hatma ya sayari ya dunia itakuwa mashakani.

Amekaribisha michango iliyotangzwa na nchi 90, zikiwemo Marekani na China, kuhusu jitihada zao za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, ambao tayari ni asilimia 80 ya utoaji wote wa gesi chafuzi duniani. Hata hivyo ametoa wito kwa nchi nyingine zitoe michango yao.

Aidha amesema dola bilioni 100 zinahitajika ifikapo mwaka 2020 kwa ajili ya nchi zinazoendelea ili kuzisaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kadhalika amezingatia umuhimu wa kuleta mabadiliko kwenye mifumo ya Umoja wa Mataifa hasa Baraza la Usalama akitoa ahadi kwamba Ufaransa haitatumia tena haki ya kupinga maazimio ya Baraza hilo kwenye hali ya mauaji ya wengi.