Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makubaliano kuhusu nyuklia Iran ni ushindi dhidi ya vita- Rais Rouhani

Makubaliano kuhusu nyuklia Iran ni ushindi dhidi ya vita- Rais Rouhani

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hassan Rouhani, amesema leo kuwa makubaliano yaliyosainiwa baina ya Iran na Marekani, Uchina, Ufaransa, Urusi, Uingerereza, EU, na Ujerumani kuhusu mpango wa nyuklia nchini mwake (JCPOA), ni mfano bora wa ushindi dhidi ya vita.

Rais Rouhani amesema hayo akilihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika mjadala wa wazi leo Jumatatu Septemba 28, akiongeza kuwa makubaliano hayo yameondoa wingu la uhasama na tishio la vita vingine Mashariki ya Kati.

Aidha, amesema kuwa mashauriano kuhusu makubaliano hayo ya nchi saba pamoja na EU, yalichukuwa muda na rasilmali nyingi, na hivyo basi juhudi zinapaswa kuwekwa katika kuyatekeleza.

Tunaamini utimizaji wa ahadi za pande zote katika makubaliano hayo ni muhimu katika mchakato wa kuyatekeleza. Sambamba na utekelezaji wa JCPOA, tunatarajia pia nchi zinazomiliki silaha za nyuklia zichukue hatua stahiki kutimiza ahadi zao za kuondoa silaha za nyuklia, kwa misingi ya aya ya sita ya Mkataba wa Kutoeneza Silaha za Nyuklia.”

Kwa mantiki hiyo, ameeleza matarajio yake kuwa nchi hizo zitaunga mkono kutokomeza silaha za nyuklia katika eneo la Mashariki ya Kati.