Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mateso na mauaji vyashamiri Burundi, watu 134 wameuawa tangu Aprili: Kamishna Zeid

Mateso na mauaji vyashamiri Burundi, watu 134 wameuawa tangu Aprili: Kamishna Zeid

Kumekuwepo na ongezeko la matukio ya watu kukamatwa, kushikiliwa na hata kuuawa nchini Burundi, jambo ambalo limemtia hofu kubwa Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Katika taarifa yake ya leo, amenukuliwa akisema kuwa tangu mwezi Aprili watu 134 wameuawa nchini humo sambamba na visa vya watu kutiwa korokoroni ambapo kwa mwezi huu pekee watu 704 wamekamatwa.

Amesema hali inayoendelea Burundi inatia woga mkubwa miongoni mwa raia kwani karibu kila siku maiti za watu zinaonekana zinazagaa kwenye mitaa ya viunga vya mji mkuu Bujumbura, na maiti wengine wakiwa na ishara za kuteswa na mikono kufungwa nyuma.

Halikadhalika Kamishna Zeid amezungumzia wasiwasi wake kuhusu hali ya watoto 52 wanaoshikiliwa sambamba na watu wazima kwenye gereza la Rumonge ambapo ametaka serikali kuwahamishia kwenye kituo cha jirani cha kuliemisha watoto.