Skip to main content

Mashambulizi dhidi ya raia Bangui yakomeshwe:OCHA

Mashambulizi dhidi ya raia Bangui yakomeshwe:OCHA

Mratibu wa misaada ya kibinadamu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR Marc Vandenberghe, amelaani mashambulizi mapya dhidi ya raia mjini Bangui mnamo Septemba 26 na kutaka pande kinzani kuheshimu sheria za kimataifa na kulinda raia.

Taarifa ya ofisi ya kuratibu misaada ya kibinadmau OCHA nchini CAR inasema kuwa mapigano hayo yalizuka baada ya kifo cha kijana Muislamu mpanda pikipiki ambapo wengi wamekufa na kujeruhiwa, nyumba zimeporwa huku nyingine zikichomwa.

Kwa mujibu wa OCHA maelfu ya watu wamekimbia makwao kusaka hifadhi ambapo Mkuu huyo wa OCHA nchini CAR ameelezea kuskitishwa kwake na idadi ya watu waliokufa na majeruhi, uchomaji wa nyumba na wimbi jipya la wakimbizi.

Bwana Vandenberghe ametuma salamu za rambirambi zake kwa familia za waathiriwa na kuwatakiwa uponyaji mwema majeruhi.  Mjini Bangui kuna vituo 30 vyenye wakimbizi zaidi ya 27,000 idadi hii ikiwa ni kabla ya mapigano ya Septemba 26.