Dunia ni lazima ichukue hatua sasa, bila kumwacha yeyote nyuma- Obama

Dunia ni lazima ichukue hatua sasa, bila kumwacha yeyote nyuma- Obama

Rais Barrack Obama wa Marekani, amesema leo kuwa ufanisi uliopatikana katika kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia yanaleta fahari, lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya.

Rais Obama amesema hayo akihutubia viongozi wa dunia kwenye Umoja wa Mataifa, katika mkutano wa Maendeleo Endelevu, SDGs. Obama amesema kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia kama vile kupunguza viwango vya njaa na umaskini duniani pamoja na vifo vitokanavyo na Ukimwi, malaria na kifua kikuu, kunaonyesha kuwa inawezekana kutimiza malengo ya maendeleo endelevu.

Kuwekeza katika afya ya umma kunazaa matunda. Tunaweza kuvunja mzunguko wa umaskini. Watu na mataifa yanaweza kuinuka katika maendeleo. Licha ya majanga ya dunia yetu na madhara ya maogonjwa, mamilioni ya maisha yanaweza kuokolewa, iwapo tutamakinika, na ikiwa tutafanya kazi pamoja.”

Akizungumza kuhusu malengo mapya ya maendeleo endelevu, SDGs, Obama amependekeza njia za kuyatimiza malengo hayo.

“Tunapaswa kujifunza kutoka siku zilizopita, tuone tulipofanikiwa, ili tuongeze maradufu ufanisi huo, na kuelewa upungufu wetu ili tuurekebishe. Na tunaanza kwa kuelewa kuwa aya hii mpya ya maendeleo haiwezi kuwa tena mhanga wa migawanyo ya zamani kati ya nchi zilizoendelea na nchi zinazoendelea. Umaskini na utofauti unaoongezeka upo katika nchi zetu zote, na nchi zetu zote zina kazi ya kufanya, ikiwamo Marekani.”

Hata hivyo, Obama amesema ni lazima kushughulikia mambo fulani ambayo ni sehemu ya maendeleo

Mosi, maendeleo yanatishiwa na uongozi mbaya. Maendeleo na ukuaji wa uchumi endelevu na jumuishi, yanategemea serikali na taasisi zinazowajali watu wao, zinazowajibika, zinazoheshimu haki za binadamu na kuwezesha haki kwa kila mtu na siyo kwa watu wachache tu. Kwa hiyo katika muktadha wa ufisadi na uporaji wa mabilioni ya pesa kutoka kwa shule, hospitali na miundombinu na kuzipeleka akaunti za benki ng’ambo, serikali zinapaswa kuendeleza uwazi na utawala wa sheria.”