Viongozi waelezea azma yao kukamilisha mkataba wa tabianchi unaofaa nchi zote

Viongozi waelezea azma yao kukamilisha mkataba wa tabianchi unaofaa nchi zote

Viongozi wa dunia wameelezea azma yao leo kukamilisha mkataba wa kudumu na wenye maana kuhusu tabianchi mjini Paris, Ufaransa, na ambao utazifaa nchi zote.

Hayo yametangazwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, akikutana na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja huo mjini New York, ambako mkutano kuhusu malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, unaendelea.

Bwana Ban amesema, katika mkutano huo wa viongozi wa dunia kuhusu tabianchi, hoja tatu zimeibuka, na ambazo zinapaswa kugeuzwa kuwa vitendo Mosi, amesema Mkataba wa Paris utapaswa kuwa wa kina, na mtazamo wa muda mrefu wa dunia iliyokombolewa kutoka kwa umaskini kupitia mabadiliko yatakayohakikisha mustakhbali wenye uchafuzi mdogo na thabiti.

Na pili:

“Mkataba wa Paris ni lazima uwe wakati wa mapinduzi, unaotuma ujumbe bayana kwa umma na sekta binafsi kuwa mabadiliko ya uchumi wa dunia hayakwepeki, yana manufaa na tayari yameanza. Viongozi wameunga mkono mkataba wa kudumu utakaoongeza kasi ya uwekezaji katika nishati safi na kuchagiza mabadiliko ya kimataifa katika uzalishaji mdogo wa gesi chafuzi kabla ya mwisho wa karne, kwa kufuata mwongozo wa nyuzi-joto mbili.”

Aidha, Ban amesema viongozi wameafikiana kwamba mkataba huo ni lazima uimarishe uhimili wa athari za tabianchi, ukiangazia watu maskini zaidi na walio hatarini zaidi. Na tatu:

“Hatua za mara moja madhubuti na za ushirikiano ni muhimu kutimiza ndoto ya mtazamo huu wa muda mrefu. Nimefurahi kusikia viongozi wakiahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuondoa vizuizi vya kisiasa.”

Katika muktadha wa malengo ya maendeleo endelevu, Ban amesema ni lazima viongozi waendeleze msukumo wa kupitishwa kwa malengo hayo kwa kuafikia mkataba imara mjini Paris mwezi Disemba.