Serikali yangu inaahidi kuhakikisha usawa wa jinsia- Rais Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, amesema leo kuwa serikali yake itaendelea kuwa imara katika kuhakikisha usawa wa jinsia na kuwawezesha wanawake.
Rais Kenyatta amesema hayo wakati wa mkutano uliowaleta pamoja viongozi wa dunia kutoa ahadi za kuchukua hatua kuhakikisha usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake.
Bwana Kenyatta amesema serikali yake itaendeleza ufanisi uliopatikana kwa wanawake chini ya katiba mpya imara, kwa kupitisha sheria mwafaka na utungaji sera, pamoja na kuzitekeleza ili kuwezesha kutimiza lengo la usawa wa jinsia.
“Tunaahidi pia kuwekeza rasilmali za kutosha kupigania usawa wa kijinsia, na kuimarisha mikakati inayojikita kwa masuala ya jinsia, na bajeti zinazojali usawa jinsia, pamoja na kuendeleza vigezo vya maendeleo ya jinsia zote na usawa.”
Aidha, Rais Kenyatta ametoa ahadi kuhusu ajira na mishahara kwa wanawake
“Serikali yangu itaendelea kushughulikia suala wa wanawake kupata ajira zenye hadhi na kushughulikia pengo la mishahara kijinsia.”
Aidha, Bwana Kenyatta ameahidi kuwa serikali yake itaharakisha utekelezaji wa sera ya kitaifa kuhusu kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia, na sheria ya kuzuia ukatili wa majumbani, na kuendelea kuwahusisha wanaume na wavulana, kulingana na kampeni ya He4She.
Kuhusu ukeketaji na ndoa za utotoni:
“Serikali yangu inaendelea kuahidi kutokomeza desturi zote zenye madhara, zikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni”