Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

"Watalii bilioni moja, fursa bilioni moja," ndio ujumbe wa Siku ya Utalii

"Watalii bilioni moja, fursa bilioni moja," ndio ujumbe wa Siku ya Utalii

Leo Septemba 27 ikiwa ni Siku ya Utalii Duniani, Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa  Ban Ki-moon, amesema kwamba siku hii inamulika uwezo wa utalii katika ulimwengu kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Huku watalii bilioni moja wa kimataifa wakisafiri duniani kila mwaka, utalii ni sekta iliyo na uwezo wa kubadili maisha ya mamilioni ya watu.

Bwana Ban amesema kwamba nafasi ya sekta hii katika maendeleo endelevu ni kubwa kwani ni miongoni mwa sekta inayoajiri watu wengi na kuwapa watu fursa na hivyo kusaidia katika kukabiliana na umaskini  na kuimarisha maendeleo jumuishi.

Kadhalika Katibu Mkuu ameongeza kwamba sekta ya utalii ni muhimu katika kuimarisha uelewa wa kitamaduni na umuhimu wa kuhifadhi tamaduni na urithi wa kitaifa kwa sababu unakutanisha watu mbali mbali.

Kwa mantiki hiyo Ban ametoa wito wa kufanya kazi pamoja ili kuimarisha sekta ya utalii na kuchagiza ukuaji wa uchumi, ulinzi wa mazingira na kuimarisha maendeleo endelevu na maisha yenye utu kwa wote.